Powered By Blogger

Alhamisi, 8 Februari 2024

NILAUMU MACHO YANGU LYRICS




Moyo umesalitika, na sababu macho yangu, Tena nnafedheheka, kupenda kitu si changu, Mwisho ntaadhirika, kupoteza pendo langu, Nilaumu macho yangu, au moyo nambieni.

Umeuliza suali, jawabu nakuletea,
Uamuzi wa halali, hukumu iso hatia,
Itakuwa ni muhali, kimoja kukionea,
Laumu vyote viwili, usilaumu kimoja.

Na moyo hausikii, umeshitadi wenzangu, Wala haujizuwii, ukaficha siri yangu, Bali wafanya bidii, upoteze roho yangu, Nilaumu macho yangu, au moyo nambieni.

Jicho hufanya idili, mzuri kumvumbua,
Na moyo bila suali, apendae huchagua,
Nawe ufurahi kweli, mapenzi kuyachukuwa, Laumu vyote viwili, usilaumu kimoja.

Macho yangu yamenena, lawama hizi si zangu, Mimi kweli nimeona, hazifumba mboni zangu, Moyo subira hauna, niutendeje wenzangu, Nilaumu macho yangu, au moyo nambieni.

Macho ndio ya awali, matatani kukutia,
Moyo ukawa wa pili, lawamani kuingia,
Moyo hauna akili, jicho halina pazia,
Laumu vyote viwili usilaumu kimoja.

Wa kumshauri sina, nikampa siri yangu,
Yareti angeniona, akajua hali yangu,
Nakufa huku naona, na sababu macho yangu, Nilaumu macho yangu, au moyo nambieni.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni